TAARIFA KWA UMMA
KINANA, CCM WANAPANGA NJAMA ZA KUMVUA LISSU UBUNGE
MAHAKAMANI!!!
Dar es Salaam, 31 Mei 2013...
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kimelaani vikali njama za Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
Abdulrahman Kinana kufufua kesi ya uchaguzi dhidi ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Mh. Tundu
Lissu. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr.
Wilbroad Slaa amedai kwamba CHADEMA imekamata nyaraka zinazoonyesha kwamba
Katibu Mkuu wa CCM Kinana amewaelekeza waliowakuwa mawakili wa makada wa CCM
waliomfungulia Mh. Lissu kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge katika
Jimbo la Singida Mashariki mwaka 2010 wafungue rufaa katika Mahakama ya Rufaa
ya Tanzania ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyotupilia
mbali kesi ya makada hao wa CCM dhidi ya Lissu. Kesi ya Mahakama Kuu
ilitupiliwa mbali tarehe 27 Aprili mwaka jana.
Dr. Slaa alisema kwamba lengo la
njama za Kinana na CCM ni kuhakikisha kwamba Mh. Lissu anafutiwa Ubunge ili
asiweze kushiriki katika mchakato wa Katiba Mpya kama mjumbe wa Bunge Maalum la
Katiba litakalojadili na kupitisha rasimu ya Katiba Mpya baadaye mwaka huu. Dr.
Slaa alisema: “Kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni na Mbunge, Mheshimiwa Lissu amekuwa mwiba mkali kwa CCM na
Serikali yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Amefumbua macho ya mamilioni ya
Watanzania kuhusu masuala makubwa ya kikatiba na kisheria kwa hoja zake
Bungeni. Uelewa wake mpana wa masuala hayo na wa Kanuni za Bunge umekuwa
kikwazo kikubwa kwa CCM na Serikali yake pamoja na uongozi wa Bunge kupitisha
mambo yao kinyume cha sheria, Kanuni za Bunge na maslahi ya nchi yetu. Uwepo
wake ndani ya Bunge na ujasiri wake katika kutetea hoja mbali mbali umemzuia
Spika wa Bunge na uongozi mzima wa Bunge kuwaonea Wabunge wa Upinzani na hasa
CHADEMA. Mtu huyu amekuwa adui mkubwa wa CCM ndio maana Kinana anataka
aondolewe Bungeni ili asiwepo kabisa katika mjadala wa Katiba Mpya Bungeni.”
Kwa mujibu wa Dr. Slaa, mara baada ya
Mh. Lissu kuwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya bajeti
ya Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 3 mwezi huu ambapo aliishambulia Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na CCM kwa kuvuruga mchakato wa uundaji wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya kwa lengo la kuhakikisha Mabaraza hayo yanakuwa ya wanachama
wa CCM tu, Kinana alimwita wakili wa kujitegemea Godfrey Wassonga wa kampuni ya
mawakili ya Wassonga Associates Advocates ya mjini Dodoma na kumwelekeza
afungue rufaa dhidi ya Lissu katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania haraka
iwezekanavyo. Siku nne baadaye yaani tarehe 7 Mei, 2013, Wakili Wassonga
alifungua rufaa hiyo katika Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
mjini Dodoma.
Ijapokuwa rufaa hiyo inaonyesha
kufunguliwa na Shabani Itambu Selema na Paschal Marcel Hallu waliokuwa
walalamikaji katika kesi iliyotupwa na Mahakama Kuu, Dr. Slaa alidai kwamba
watu hao hawahusiki kwa namna yoyote ile na kufunguliwa kwa rufaa hiyo.
“CCM na mawakili wao wanawatumia tu
wanakijiji hawa bila hata kuwapa taarifa au kuwashirikisha kwa namna nyingine
yoyote. Huyu Shabani Itambu Selema amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye
na mwenzake ambaye bado ni Katibu Kata wa CCM huko kwao, hawakuambiwa chochote
juu ya kufunguliwa kwa rufaa hiyo. Hawakutoa maagizo yoyote kwa Wakili Wassonga
kufungua rufaa kwa niaba yao dhidi ya Lissu; hawajamruhusu Wakili huyo kupinga
maamuzi ya Mahakama Kuu iliyoridhika kwamba uchaguzi wa Mbunge Lissu ulikuwa
halali; hawajamlipa Wakili Wassonga kwa ajili hiyo. Huyu Wakili anafunguaje
kesi au rufaa bila kuambiwa au kulipwa na ‘wateja’ wake? Kama huku sio kukosa
maadili ya kiuwakili ni kitu gani?”, amehoji Dr. Slaa.
Kuhusu ushiriki wa Kinana katika
sakata hilo, Dr. Slaa alisema kwamba mara baada ya rufaa hiyo kufunguliwa,
Wakili Wassonga alimwandikia Katibu Mkuu huyo wa CCM barua yenye kumbu kumbu
Na. NO/KM/CCM/01/2013 kwa ajili ya “MADAI YA MALIPO YA AWALI YA SHAURI LA RUFAA
KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI SHABANI ITAMBU SELEMA NA MWENZAKE
DHIDI YA MH. TUNDU LISSU.” Barua hiyo inamkumbusha Kinana juu ya ‘makubaliano’ kati
ya Wassonga Associates Advocates na CCM kuhusu kusimamia kesi ya wanachama hao
wa CCM dhidi ya Mh. Lissu ambayo baadae ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu.
“Baada ya shauri husika nilipata
maelekezo kutoka kwa wanasheria wa CCM kwamba tukate rufaa Mahakama ya Rufaa
kazi ambayo tumekamilisha.” Wakili Wassonga anamweleza Kinana “... katika
shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa na CCM Singida Mkoa na hawakumalizia malipo.”
Barua hiyo imeambatana na hati ya madai ya malipo (invoice) kwa ajili ya
‘malipo ya awali’ ya shilingi milioni mbili.
Dr. Slaa alidai kwamba kazi ya Lissu
na wabunge wa CHADEMA ndani ya Bunge inawatisha CCM na Serikali yake ndio maana
sasa Kinana anataka Lissu aenguliwe kwa kutumia Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
“CCM inatapatapa, Bungeni hapakaliki kwa sababu ya hoja za Lissu na Wabunge
wengine wa CHADEMA. Kila siku Bunge linaahirishwa ili kukwepa mijadala mikubwa
juu ya matukio muhimu yanayoisibu nchi yetu.
Njama za kuizima CHADEMA kwa
kuipunguzia muda wa kuzungumza Bungeni zimeshindikana; mikakati ya kuvuruga
hoja za CHADEMA kwa kuingilia hotuba za Kambi Rasmi ya Upinzani na kutaka
sehemu za hotuba hizo zifutwe zimegonga mwamba; vitisho vya Spika Makinda na
Naibu Spika Ndugai kuwasimamisha wabunge wetu hazijafua dafu. Sasa tuna taarifa
kwamba Kinana anataka kuwahonga majaji ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
mamilioni ya fedha ili wamfutie Kamanda wetu Lissu ubunge. Naye atashindwa
pia.”
Akizungumzia hati ya kiapo ya Shabani
Itambu Selema ambaye alihama CCM na kujiunga na CHADEMA baada ya kesi yao
kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu mwaka jana, Dr. Slaa amesema:
“Tutaishangaa sana Mahakama ya Rufaa
kama itaisikiliza rufaa hiyo hata baada ya aliyekuwa mhusika wa kesi ya msingi
kusema kwa kiapo kwamba yeye na mwenzake hawajakata rufaa bali ni mambo ya
Kinana na CCM yake!”
Dr. Slaa alisema itakuwa ajabu kwa
Mahakama ya Rufaa kusikiliza rufaa iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja tangu
Mahakama Kuu ilipotupilia mbali kesi ya msingi. “Kwa mujibu wa kifungu cha 115
cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mahakama ya Rufaa inatakiwa kusikiliza
rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu
rufaa ilipofunguliwa. Huyu Kinana na CCM yake wamesubiri mwaka umepita tangu
Mahakama Kuu ilipokataa kufuta matokeo ya Lissu ndio wafungue rufaa. Kama huku
sio kukanyaga spirit ya Sheria hiyo ni kitu gani?”, amehoji Dr. Slaa.
Aliongeza kuwa katika kesi ya Mbunge
wa Arusha Mjini (CHADEMA), Mh. Godbless Lema aliyekuwa anashtakiwa na wanaCCM
pia, Mahakama ya Rufaa ilipiga marufuku wapiga kura ambao hawakunyimwa haki zao
za kupiga kura kufungua malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
“Hata wino wa Mahakama ya Rufaa
katika hukumu ya Lema haujakauka Kinana na CCM yake wanataka Mahakama ya Rufaa
iyale matapishi yake kwa kusikiliza rufaa ya wapiga kura wanaodai kwa kiapo
kwamba walielekezwa na wakubwa wao katika CCM kufungua kesi iliyokataliwa na
Mahakama Kuu na sasa rufaa imefunguliwa kwa maelekezo ya Kinana bila hata wao
kujulishwa au kushirikishwa kwa namna yoyote ile," amesema Dkt. Slaa.
Dr. Slaa alisema kwamba rufaa ya sasa
inathibitisha kauli inayodaiwa kutolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya Tundu
Lissu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo Kikwete alidaiwa
kuwaambia wanaCCM mjini Singida kwamba ni afadhali Dr. Slaa achaguliwe kuwa
Rais kuliko Tundu Lissu kuwa Mbunge.
“Kwa kazi zake ndani na nje ya Bunge
Lissu amethibitisha umahiri na uzalendo wake kwa Tanzania na kwa chama chetu.
Ametetea wabunge na viongozi wetu dhidi ya njama za CCM kuwachafua kwa
kuwafungulia mashtaka ya uongo mahakamani; ametetea Watanzania kila mahali
nchini, na ameelimisha wananchi kwa hoja zake Bungeni. Ni mmoja wa Wabunge
hodari, jasiri na wachapa kazi katika Bunge hili. Huyu ndiye Mbunge ambaye
Kinana na CCM wanataka aondolewe Bungeni kwa mbinu za kishetani za aina hii.
Hatutakubali na tunawataka Watanzania wasikubali!”
Rufaa dhidi ya Lissu bado haijapatiwa
namba ya usajili licha ya kwamba imeshalipiwa ada ya kuifungulia na tayari
imeshapokelewa na Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Dodoma.
Aidha, rufaa hiyo haijapangiwa majaji wa kuisikiliza wala tarehe ya kusikilizwa
kwake haijapangwa.
---------------------------------------------------
Tumaini Makene
CHADEMA
Senior Information(Press) Officer
No comments:
Post a Comment