KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA
FEDHA 2013/2014
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika bajeti ya
wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji na kiuwajibikaji katika wizara
hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya
mambo yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1.
Kuziwezesha balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha
za kutosha ili ziweze kufanya kazi kwa
ufanisi
2.
Kutoa idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba
za mabalozi, nyumba za maafisa wa balozi na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa
idadi ya nyumba katika nchi na kama nyumba hizo zina hati miliki au la.
3.
Kutoa taarifa ya namna kila ubalozi
ulivyotekeleza sera ya Diplomasia ya uchumi kwa kuzingatia kwamba balozi nyingi
ziko hoi kifedha kiasi cha kwamba waambata wa kiuchumi wanakosa fedha za
kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili ya upelelezi wa masuala ya
kiuchumi.
4.
Kulikarabati jengo la ubalozi wa Tanzania huko
Msumbiji lililokuwa limechakaa kwa kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa
jengo hilo tulipewa bure na Serikali ya Msumbiji chini ya FRELIMO.
5.
Kujenga kitega uchumi katika kiwanja cha Tanzania kilichopo Dubai na kukiendeleza
kiwanja namba 19 tulichopewa bure na Serikali
ya Uingereza kilichopo Uingereza (Central London) ambavyo vimekuwa maficho ya
wezi kwa kutoendelezwa kwa muda mrefu na kusababisha Serikali za nchi hizo
kutaka kutaifisha viwanja hivyo.
6.
Kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za balozi zetu
nchini China, na Uingereza kutoa hati za kusafiria kwa mataifa mengine hasa ya
Afrika Magharibi ili kubaini ukweli na kuliondolea taifa aibu kutokana na
tuhuma hizi.
7.
Kukarabati jengo la ubalozi wetu nchini China
ambalo lilikuwa na nyufa na kuvuja nyakati za mvua, na kununua samani na vifaa vya ofisi kama mashine za nukushi na
za kurudufu ambazo zilikuwa hazipo,
8.
Kununua magari mapya ya ofisi ya ubalozi wetu
nchini China kwa kuwa magari matatu
yaliyokuwepoyalikuwa yameshapitiliza muda wa miaka 10 ambao kwa mujibu wa
sheria za China hayapaswi kutumika tena,
9.
Kupeleka mwambata wa kiuchumi (economic attaché) nchini China ili kufuatilia fursa mbalimbali
za kiuchumi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mahusiano
makubwa ya kibiashara kati ya nchi yetu na China
10.
Kuwawekea zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa
viongozi wa shughuli za kiserekali ili walau kuonesha uwajibikaji wa kimaadili
(moral accountability) baada ya kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa
dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
11.
Kuchunguza na kuwachukulia hatua watanzania
(wafanyabiashara na wanasiasa) waliotorosha kiasi kikubwa cha fedha za nchi
yetu (zaidi ya shilingi bilioni 315) na kuzificha katika mabenki ya uswisi
12.
Kutoa mchanganuo wa jinsi fedha za rushwa ya rada
(chenji ya rada) zilivyotumika
13.
Kueleza bayana faida za kiuchumi tunazopata kama
taifa kwa kushirikiana na jumuiya mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha
kwamba mashirikiano hayo hayatumiki kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya
“uwekezaji”
Mheshimiwa Spika, kabla
sijajielekeza kwenye mambo mahsusi kwa kipindi hiki cha bajeti ya 2013/2014,
napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA, kuitaka Serikali kutoa majibu mbele ya Bunge hili
tukufu, kwamba imetekeleza kwa kiwango gani masuala yaliyoorodheshwa hapo juu,
tuliyoitaka iyatekeleze (moja baada ya jingine) kwa mwaka wa fedha unaomalizika
wa 2012/2013?
1.1 Upotevu
wa Fedha za Safari za Rais, Shilingi bilioni
3.5
Mheshimiwa
Spika,
katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013 nilihoji kuhusu
serikali Kuchunguza na kuchukua hatua kwa waliohusika na upotevu wa shilingi
bilioni 3.5 kwa ajili ya safari “hewa” za Rais nje ya nchi, ili waweze
kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa
Spika, fedha hizi ni nyingi sana na hasa ikikukumbukwa kuwa mwaka jana 2012 wapo
mawaziri ambao walichukuliwa hatua na Bunge hili kutokana na upotevu ama
madhaifu yaliyofanyika kwenye wizara zao, wapo ambao walihukumiwa kutokana na
kupotea kwa Twiga kwenye wizara zao, wapo waliohukumiwa kutokana na udhaifu
katika kusimamia wizara zao na taasisi zilizoko chini yao. Kambi rasmi ya upinzani, inahoji iweje leo waziri aliyeshindwa
kusimamia wizara yake na kusababisha upotevu wa fedha hizi mpaka leo bado yupo,
wakati wapo mawaziri wengine walioshughulikiwa kutokana na udhaifu walioonyesha
kwenye kusimamia wizara zao, au ndio kusema kuwa Serikali hii ya CCM inafanya
upendeleo na kuonea baadhi ya mawaziri na kuwaacha wengine? “This
clearly indicates the “double standard” nature of this Government in the
performance of its functions”
1.2. Kuanzishwa kwa Ubalozi Mdogo Guangzhou -China
Mheshimiwa
Spika, mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kuwa serikali ianzishe
ubalozi mdogo katika Jiji la Guangzhou kwa ajili ya kurahisisha biashara kati
ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa serikali
imelifanyia kazi wazo hili na imeamua kuanzisha ubalozi mdogo katika mji huo
,ila tunataka kujua ni lini ubalozi huu utazinduliwa rasmi, kupata watendaji na
vitendea kazi ili uweze kuanza kufanya kazi .
2.0 DIPLOMASIA YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, moja ya
matarajio ya ushirikiano wa kimataifa ni kuweza kutafuta, na kunufaika na fursa
mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kupatikana katika mashirikiano hayo ili kama
Taifa, tuweze kujikwamua kiuchumi na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kinyume
na matarajio hayo mazuri, sasa nchi yetu imegeuzwa kuwa kitega uchumi cha nchi
zilizoendelea kwa kisingizio cha “ushirikiano wa kimataifa” chini ya
mwavuli wa “uwekezaji”. Matokeo ya
ushirikiano huu wa kinyonyaji (exploitative relationship) ni kwamba kiwango cha
umasikini katika nchi yetu kimeongezeka na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa
tegemezi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla.
Mheshimiwa Spika, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikerwa na unyonyaji na unyanyasaji uliokuwa
ukifanywa na wakoloni, hali iliyompelekea kusema maneno yafuatayo:
“Tumeonewa kiasi
cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha.
Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka
kufanya mapinduzi”
Mheshimiwa Spika,
baada uhuru, Mwalimu akaanzisha siasa ya Ujamaa na
Kujitegemea. Ujamaa ulilenga kujenga umoja wa kitaifa na umoja wa bara la Afrika dhidi ya unyonyaji
wa kibeberu, wakati kujitegemea kulimaanisha kujenga uchumi endelevu ili kulijengea taifa
heshima na nguvu ya maamuzi mbele ya mataifa mengine, na kuliepusha taifa na
fedheha ya kuombaomba.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani imesikitishwa sana na kitendo cha Serikali kulidanganya taifa, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010
kwamba: “Katika kipindi cha miaka mitano 2010 -2015, Serikali ya Chama cha
Mapinduzi itatekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi” wakati Ibara ya 98 (i) ya Ilani
hiyohiyo ya CCM inasema kwamba Serikali ya CCM itaendelea kushinikiza nchi
tajiri kutekeleza ahadi yao ya kutenga asilimia 0.7 ya pato la taifa la nchi
zao kwa ajili ya misaada kwa nchi masikini”.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba ahadi hii ya asilimia 0.7 ya pato
la taifa la nchi tajiri ambayo Serikali ya CCM inakodolea macho ni fedha za
walipa kodi wa nchi hizo kama ambavyo wananchi wetu wanavyolipa kodi. Aidha ni
aibu kwa Serikali hii ya CCM kuchukua ahadi za wahisani na kuziweka kwenye
ilani ya uchaguzi ya CCM kama ahadi kwa wananchi ili kubembelezea kura.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uvivu wa kufikiri na kubuni mbinu za
kuikwamua nchi hii na umasikini, Serikali hii ya CCM sasa hivi imeachana kabisa
na sera ya kujitegemea, ambayo Mwalimu
kupitia Azimio la Arusha alisema kwamba “ … Hakika ni ujinga na upumbavu zaidi kwetu
sisi, kufikiri kwamba tutaondokana na
umasikini wetu kwa misaada ya fedha kutoka nje kuliko rasilimali zetu wenyewe”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kulieleza bunge hili, kama inatekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutegemea ahadi
ya misaada ya fedha kutoka kwa wahisani na kama hilo ndio suluhisho la matatizo
yanayokumba uchumi wetu kama taifa kwamba tutaweza kuendelea kwa kutegemea
hisani na fadhila za wafadhili huku tukishindwa kuzitumia rasilimali zetu kwa
ajili ya kujikomboa kiuchumi.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani imejiridhisha kwamba
kauli mbiu ya ‘Diplomasia ya Uchumi’
imeendelea kubakia kama ilivyo kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’ ambayo imebakia kutamkwa na viongozi bila kuwa na
mkakati wa utekelezaji wala vigezo vya kupima kiwango cha utekelezaji wake.
3.0.
VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu
wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ‘United
Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012 iliyoandaliwa na Aili Mari Tripp ilionyesha kuwa misaada
ya wahisani kutoka nje katika mabadiliko ya kisiasa Tanzania ‘Donor
Assistance and Political Reform in Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada
kutoka nje yenye thamani ya dola za
kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka
1990-2010.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kusini mwa jangwa la
Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka nje ya nchi na hasa kutoka mataifa ya
Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza,
Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama Benki ya
Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na mengineyo. Pamoja na misaada yote hiyo, bado
tumeendelea kuwa nchi maskini sana duniani pamoja na kuwa na rasilimali lukuki
ambazo tumepewa na Mungu ila tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na
badala yake tumeendelea kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana
na rasilimali zetu kama madini, misitu
,wanyama nk kwa ajili ya misaada hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na
baadhi ya vyama vingine vya siasa katika mataifa ya magharibi na vimekuwa
vikipokea misaada ya aina mbalimbali kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya
makubaliano na mirengo ya kiitikadi ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado
vipo vyama vya siasa vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea
kutoka nje ya nchi na vyama hivi vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za
uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Spika, CCM
wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na wamekuwa wakipokea
misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka Umoja wa Vyama vya Kikomunisti
Ulimwenguni ‘Socialist International’ kutoka katika nchi kama za
Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha Labour,China kupitia chama
cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha Democrats. Pamoja na misaada ya
kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi
hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo
kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali
ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia
moja, usagaji na ushoga”. Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye
mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa
Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha
Liberal Democrats wakati chama hicho(www.liberal-international.org) kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu
ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya
Canada, Det Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal
Group cha Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana
na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine
mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali na msaada wa mwisho
ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na chama cha Kiliberali
kutoka Norway.
Mheshimiwa Spika, kwa upande
wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia
Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu ni umoja wa
vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake mkuu ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi
muhimu katika jamii, ikimaanisha kwamba: “tunapinga
vitendo vyote vya ushoga na usagaji”. Tunatetea demokrasia, haki za binadamu na kupambana na
ufisadi katika serikali. Vyama wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative
Party cha UK, CPP cha Norway, Republican cha Marekani na vingine
vinavyofuata mrengo huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani
Bungeni, inavitaka vyama vyote ambavyo vimekuwa na mahusiano na vyama
vya nje viweke wazi mikataba yao na malengo ya mahusiano hayo ikiwa ni pamoja
na misaada ambayo vimekuwa vikipokea kutoka kwenye nchi hizo .
4.0 MPANGO WA
KUJITATHIMINI KIUTAWALA BORA (APRM)
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Januari, 2013
ulifanyika mkutano wa 20 wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini
Addis Ababa ,Ethiopia na ni katika mkutano huo Mhe. Rais Kikwete aliwasilisha
taarifa ya nchi yetu kuhusu kujitathimini katika utawala bora kwenye mpango wa
nchi zinazojitathimini katika utawala bora (APRM).
Mheshimiwa Spika, baada ya taarifa hiyo (randama uk.15) nchi yetu
ilitakiwa kutafutia ufumbuzi changamoto zifuatazo;
i.
Migogoro baina ya
wakulima na wafugaji
ii.
Imani za kishirikiana
(uchawi)
iii.
Kuhakikisha kuwa
manufaa ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi
iv.
Kutoa elimu kwa umma
kuhusu mipango na sera za serikali
Mheshimiwa Spika, changamoto hizi ambazo nyingine zinatia aibu
taifa letu mbele ya mataifa mengine kama vile sisi kuonekana ni wachawi na
hivyo kutakiwa kuchukua hatua dhidi ya uchawi !ni fedheha na aibu kubwa kwa
taifa letu .
Aidha , Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inataka
kujua serikali na wizara imechukua hatua gani mpaka sasa katika kukabiliana na
changamoto hizi na hasa tatizo la wakulima na wafugaji na kuhakikisha kuwa
manufaa ya kukua kwa uchumi wetu yanawanufaisha wananchi na sio kuwanufaisha
baadhi ya viongozi na mafisadi wachache.
5.0 MLIPUKO WA
BOMU ARUSHA NA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu tarehe 05 Mei, Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti huko Arusha lililipuliwa kwa bomu.
Tukio hili lilitokea wakati akiwepo balozi wa Vatican Nchini na ambaye
ndio alikuwa mgeni wa heshima kwenye tukio la kuzindua Parokia hiyo.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya tukio hilo, Balozi wa Vatican nchini
aliwasilisha taarifa hiyo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na
kuonyesha kuwa Tanzania sio nchi salama sana kutembelewa na wageni na kama
wakitembelea basi wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa kipindi chote watakapokuwa
hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua nini kauli ya serikali
kuhusiana na tukio hili na hasa kuhusiana na taarifa za hali ya usalama wa nchi
yetu na wageni zilizowasilishwa kwenye Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa .
6.0 SAFARI ZA VIONGOZI NJE NA MISAFARA
MIKUBWA
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka
2011/2012 Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji suala la misafara ya
Viongozi wa kitaifa kuwa mikubwa kutokana na kuambatana na watu wengi ambao
wengine wanakuwa hawana hata majukumu ya
msingi ya kufanya wakati wa ziara hizo huku wakiliongezea taifa gharama kubwa
ya kuwasafirisha na na kulipia malazi yao na starehe zao.
Aidha ,
tumekuwa tukipendekeza na kushauri kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Rais wa nchi
kuamua kutuma wasaidizi wake kwenye baadhi ya ziara za nje kama wanavyofanya
viongozi wengine wa nchi jirani kama Rais Kagame wa Rwanda na hata Mwai Kibaki, Rais mstaafu wa Kenya alivyokuwa anafanya
akiwa Rais, kwani kwa kufanya hivyo
atapunguza msururu wa maafisa na viongozi mbalimbali wa kuambatana naye.
Tunashauri tena kuwa rais awe anatuma wasaidizi wake kwenye ziara za kawaida na
yeye awe na jukumu la kushiriki kwenye ziara rasmi za kiserikali ‘State
Visits’ na mikutano maalum ya Kimataifa kama UN na AU.
Hivyo
basi Kambi rasmi ya Upinzani inashauri mambo yafuatayo yafanyike ili kupunguza
gharama hizi kubwa za kuwasafirisha viongozi na misafara isiyokuwa na tija kama
ifuatavyo;
i.
Serikali itengeneze kanuni za kuthibiti idadi ya
maafisa na watu ambao watakuwa wakiambatana na Rais kwenye ziara za nje (idadi
ya wajumbe kwenye misafara iwe wazi na ijulikane)
ii.
Pawepo na kanuni za kuainisha kuwa ni nani
watapaswa kupanda ndege daraja la kwanza na wale wenye haki ya kulala kwenye
hoteli za daraja la kwanza wajulikane.
6.1. Idara
ya Protocol na Mabilioni ya Fedha za Safari za Nje.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2011/2012 fungu 221100 ‘travel out of country’zilitumika
shilingi 36,121,942,870.00 kwa ajili
ya safari za nje ya nchi kwa viongozi wakuu. Katika mwaka wa fedha uliopita wa
2012/2013 kifungu 1010 ambacho ni kwa ajili ya protocol walitengewa shilingi 8,372,581,824 na fedha ambazo zilikuwa
zimepokelewa na wizara mpaka mwezi Februari 2013 zilikuwa jumla ya shilingi 26,081,860,727.16! (randama uk.4)jedwali
la 2 na zilitumika kwa ajili ya kugharamia safari za viongozi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2012/2013 Bunge lilikuwa limetenga na kuidhinisha kiasi cha
shilingi 8,372,581,824 kwa ajili ya
kifungu hiki cha Protocol ‘travel out of Country’kwa mujibu wa kitabu cha
matumizi ya kawaida juzuu ya pili (volume II). Jambo la kushangaza ni kwamba, wizara iliieleza kamati na Bunge hili kuwa
walishatumia zaidi ya bilioni 26.081 kutokana na fedha walizokuwa wamejitengea
wenyewe wizara ambazo hazikuidhinishwa na Bunge kiasi cha bilioni 29.404
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi
ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA,
inataka maelezo ya kina kuhusiana na mamlaka ya wizara hii kwenda kutenga na
kutumia fedha nyingi kuliko zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili na zilikuwa
fedha kwa ajili ya safari za kwenda nje ya nchi, ni nani aliipa wizara mamlaka
hiyo na kiburi hicho kiasi cha kupuuza maamuzi ya Bunge hili tukufu.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka huu wa fedha 2013/2014 kitengo hiki cha Protocol kimetengewa jumla ya
shilingi 15,155,377,400.00 kwa ajili
ya matumizi mengineyo ,ambazo katika
mchanganuo wake kwenye kifungu 1010 kifungu kidogo cha 221100 ‘travel out of
Country’ zimetengwa shilingi 9,381,328,850.00
kwa ajili ya kugharamia safari za kikazi za viongozi wa Kitaifa nje ya nchi.
Aidha,
katika kifungu kidogo cha 220700 ‘rental expenses’ zimeombwa jumla ya shilingi 2,925,445,000.00 kwa ajili ya kukodisha
ndege ,magari na kumbi za mikutano kwa ajili ya viongozi wa kitaifa.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani
na kamwe haitakubaliana na ufujaji huu wa fedha za walipakodi maskini wa
Tanzania . Tunamtaka waziri atoe maelezo ya kina kwa watanzania ni kwanini nchi
maskini kama yetu tutumie fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya safari za viongozi
nje ya nchi? Aidha , hatukubaliani na kitendo cha kutenga fedha kwa ajili ya
kukodi ndege wakati Rais ana ndege yake ambayo ilinunuliwa na
mabilioni ya fedha za watanzania. Ikumbukwe kwamba ndege hii ya Rais
ilinunuliwa kwa mbwembwe nyingi kiasi kwamba Waziri wa Fedha wa wakati huo
Ndugu Bazili Mramba alisema watanzania wafunge mkanda, hata kama watakula
majani, lazima ndege ya Rais inunuliwe. Watanzania hawa wamekula majani sasa
kiasi cha kutosha, bado tena Serikali inaendelea kuwanyonya ili ipate pesa za
kukodisha ndege wakati Rais ana ndege? Hivi Serikali sasa inataka watanzania
wale mawe ndio ijue kwamba watu wamefunga mkanda kiasi cha kutosha?
6.2 Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje
Mheshimiwa Spika, mwaka
2012 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, ilifanya
ziara kwenye balozi takribani zote na iliona matatizo yanayozikumba balozi zetu
huko na ilikuwa matumaini yetu kuwa baada, ya ziara ile ya kamati ingehakikisha kuwa fedha zinaongezwa kwenye
wizara hii na hasa kwenye fungu la maendeleo ili tuweze kuboresha mazingira ya
balozi zetu. Kinyume na matumaini hayo, ni kwamba hakuna jitihada zilizofanyika
kuongoeza bajeti ya wizara hasa katika fedha za maeendeleo.
Mheshimimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, inaitaka kamati ya Bunge ya Ulinzi na usalama,
kuishinikiza Serikali ili kuhakikisha
kuwa katika mwaka huu wa fedha wizara hii inaongezewa fedha kwa ajili ya
kuboresha mazingira ya balozi zetu , na hiyo ndio njia pekee ya kuonyesha kuwa
kamati haikuenda kufanya utalii bali ilienda kuona matatizo ya balozi zetu na
kuchukua hatua.
7.0 UFISADI KATIKA UNUNUZI WA JENGO LA OFISI
NA MAKAZI KATIKA UBALOZI WA TANZANIA JIJINI PARIS – UFARANSA.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka huu wa fedha kwa mujibu wa randama ya wizara
ni kuwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 28 (28,000,000,000.00)
zimepangwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na kati ya hizo kiasi cha
shilingi bilioni 24 na milioni 188 (24,188,000,000.00) ni kwa ajili ya
ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya balozi jijini Paris ,Ufaransa (randama
uk 25) na kiasi cha shilingi bilioni 3
na milioni 812 (3,812,000,000.00) ni kwa ajili ya gharama za ukarabati wa
majengo ya ofisi na makazi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika,
ukisoma randama ya wizara (uk.120) katika kasma 6391 ,kifungu kidogo 411100
kiasi cha fedha kilichoombwa ni shilingi
bilioni 23 na milioni 900 (23,900,000,000)
kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya Balozi jijini Paris, Ufaransa
na shilingi bilioni 3 namilioni 700 (3,700,000,000.00)
kinaombwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi yaliyopo
ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Hata
hivyo, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kwenye kasma 6391 katika fungu la
Maendeleo (randama uk.120) wizara inaomba kutengewa kiasi cha shilingi milioni 400 (400,000,000.00) (kifungu
221100 ) fedha ambazo hazipo kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida juzuu ya
pili (volume II) kwa ajili ya posho ya kujikimu na gharama za usafiri kwa ajili
ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara, miradi yenyewe ni
miwili mmoja wa kununua nyumba Ufaransa na kukarabati jengo Msumbiji.
Mheshimiwa Spika,
mkanganyiko huu wa kimahesabu unatia mashaka makubwa sana kuhusiana na dhamira
ya serikali na wizara hii hasa fedha zinapotengwa bila kufuata utaratibu wa
kibajeti na bila kuingizwa kwenye vitabu vya fedha na mafungu husika.
Kambi rasmi ya Upinzani,
inajiuliza tunapitisha mafungu yapi? Kwani kwenye randama fedha zinatofautiana
kwenye fungu moja la maendeleo baina ya (ukurasa 25 na 120) , vilevile kwenye
kitabu cha matumizi ya kawaida hali ni tofauti kwenye fungu la travel out of the Country kwani sasa
wizara imejiongezea shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kufuatilia miradi
miwili ambayo ni kununua jengo Paris na kukarabati Jengo la ubalozi - Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, utata
wa fedha unaendelea kuonekana kwenye randama ya wizara katika kiambatanisho
Na.1 ‘utekelezaji wa ushauri na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge ya
mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa’ katika ushauri/mapendekezo Na.5
kamati iliitaka ‘Wizara itoe mchanganuo wa matumizi ya fedha za bajeti ya
maendeleo zilizopokelewa kutoka hazina katika mwaka wa fedha 2012/13’
Maelezo
ya wizara yalikuwa kama ifuatavyo; nanukuu randama ya wizara “katika mwaka wa fedha 2012/2013 ,hadi
kufikia mwezi Machi ,2013 wizara imepokea kutoka Hazina kiasi cha shilingi 13,261,281,600.00 ambapo kati ya fedha
hizo kiasi cha shilingi 9,660,000,000.00
zimetumika kwa ajili ya kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa Jengo la Ofisi na
Makazi ya Balozi Paris,Ufaransa;shilingi 995,930,000.00
zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa jengo la serikali lililopo Maputo,Msumbiji
;shilingi 626,899,155.00 zimetumika
kwa ajili ya ukomboaji wa vifaa vya ujenzi bandarini vilivyotumika katika ujenzi
wa kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere na safari ya kikazi ya
wataalam katika balozi za Maputo,Pretoria na Lusaka kwa ajili ya kazi ya
upembuzi yakinifu wa miradi ya maendeleo iliyopo katika Balozi hizo; na
shilingi 1,978,452,485.20 bado
hazijatumika na zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kulipia gharama za ukarabati
wa jengo la Serikali lililopo Maputo’
Mheshimiwa Spika, baada ya kufuatilia na kufanya
tathimini ya kina kuhusiana na majibu hayo ya wizara kuhusu fedha za maendeleo
kwa ajili ya ukarabati wa Jengo la Maputo na kununua Jengo la Ofisi na Makazi
ya Balozi Ufaransa na kukuta kuwa ni fedha nyingi sana kuliko uhalisia wenyewe
, kwa mfano waziri anataka Bunge na taifa tuamini kuwa kufanya ukarabati wa
jengo moja la ofisi Maputo Msumbiji tunahitaji kutumia kiasi cha shilingi 4,695,930,000.00 kwa kutumia fedha
inayoombwa mwaka huu wa fedha na zile ambazo tayari zilishalipwa katika mwaka
wa fedha wa 2012/2013. Aidha wakati wizara inawasilisha majibu yake kwenye
kamati ya kudumu ya Bunge walisema kuwa (swali 12 uk.5) ‘kiasi
cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo
Maputo ni shilingi 3,812,000,000.00……kiasi hicho cha fedha kinatosheleza
kukamilisha kazi ya ukarabati wa majengo hayo ya Serikali yaliyopo Maputo, Msumbiji’
Aidha, kununua
jengo moja la ofisi na makazi katika Jiji la Paris Ufaransa tunahitaji kutumia
kiasi cha shilingi bilioni 33 na milioni
560 33,560,000,000.00.
Mheshimiwa Spika, kwa
majibu haya ya wizara ni kuwa tayari wizara imeshafanya malipo ya shilingi bilioni 9.66 kama malipo ya awali kwa
ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi huko Paris Ufaransa , na kuwa
tayari tumeshafanya malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 995.930 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ubalozi huko
Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, hakika
kiasi hiki ni kikubwa kupitiliza na hata utafiti na tathimini ambayo ilifanywa
na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha kuwa kununua jengo la ofisi
katika jiji la Paris kwenye mji wa bei ghali kama Co’te d’Azur (most expensive area in Paris) huwezi kutumia fedha
nyingi kiasi hicho kwa ajili ya manunuzi ya jengo la ofisi na makazi.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunakumbuka sakata la ununuzi wa jengo la
ubalozi lililomkumba balozi Prof.Mahalu huko Roma - Italia na yaliyofuatia
mpaka kesi na fedha zetu tulizoambiwa kuwa zimepotea hazikuweza kurejeshwa
baada ya Prof.Mahalu kushinda kesi hiyo mahakamani.
Hivyo basi,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu kuhusiana na mambo
yafuatayo;
i.
Ni eneo gani ambalo tumepata jengo la kununua kwa
ajili ya ubalozi na makazi ya balozi huko Paris, Ufaransa, na ni nyumba ya aina
gani .
ii.
Je, Serikali inaweza kuonyesha mkataba wa
manunuzi wa nyumba hizo (Paris) kwa Bunge na tutalipa kiasi gani kununua jengo
hilo?
iii.
Ni nani au wakala gani wa serikali aliyefanya
tathimini ya hayo majengo na kuamua kuwa tulipe kiasi hicho cha fedha?
iv.
Ni kampuni gani iliyohusika katika kufanya
makubaliano ya mauziano ya nyumba hizo na tunawalipa kamisheni ya shilingi
ngapi?
v.
Nani, aliidhinisha kutumika kwa kiasi kikubwa
hivyo kwa ajili ya kununua jengo la Ubalozi na makazi huko Paris, je Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, ilishirikishwa katika manunuzi haya?
vi.
Ukarabati unaofanywa kwenye jengo la Maputo
Msumbiji ni wa aina gani, au tunajenga upya nyumba hizo?
vii.
Ni kampuni gani ya ujenzi inayofanya ukarabati wa
jengo letu huko Msumbiji na mkataba wa ukarabati huo uko wapi, tungetaka uwekwe
hadharani.
Aidha , kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ,
inatoa hoja ya kumtaka Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi maalum (Special Audit)
kuhusiana na ununuzi wa majengo haya na ukarabati unaofanyika kwenye jengo letu
huko Maputo, Msumbiji, na kuona kama thamani halisi ya fedha imezingatiwa , na
kama sheria ya manunuzi ya umma imefuatwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Vile vile,
tungetaka sehemu ya fedha hizi zitumike kwa ajili ya kukarabati jengo letu la
zamani la ubalozi lililopo Washngton ambalo kwa sasa halitumiki baada ya
kutekelezwa kwani likikarabatiwa litaweza kuliongezea taifa mapato kutokana na
matumizi ya kibiashara ya jengo hilo.
8.0 MPANGO WA WIZARA WA KUTOA VISA KWENYE
BALOZI TU
Mheshimiwa Spika, mpango
wa Wizara kutoa visa kwenye balozi tu haukubaliki. Kwa Mujibu wa majibu ya wizara kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya
Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ilionyesha kuwa ili wizara iweze
kukusanya fedha za kutosha kwenye balozi zetu ni kwa kurudisha utaratibu wa
utoaji wa viza kufanywa na Balozi zetu tofauti na utaratibu unaotumika hivi
sasa ambapo wageni huweza kupatiwa viza pindi wanapowasili katika vituo vya kuingilia nchini (viza on
arrival).
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
haikubaliani na wazo hili la wizara kwani badala ya kuongeza wageni kuja nchini
litapunguza sana hasa ikizingatiwa kuwa ni nchi chache sana ambako tuna ofisi
za Balozi na pia kuna nchi nyingine kama Marekani ambapo, kama mgeni yupo
Carlifonia na anataka kusafiri kuja Tanzania atalazimika kwanza kusafiri kwenda
Washington ambako ndiko kwenye ubalozi atafute visa na ndipo aweze kuja nchini.
Utaratibu huu utaongeza gharama kubwa za
usafiri kwa wageni na watalii na hivyo kulipotezea taifa mapato yataokanayo na
utalii kwani wageni watapungua.
Aidha,
tunaikumbusha wizara kuhusiana na Itifaki ya kuwa na“Single Tourist Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria
na visa moja ya utalii “Single Tourist Visas”
kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kama sisi tukifanya huo uamuzi basi
wenzetu Kenya wataendelea kupata wageni wengi zaidi kutokana na visa ya pamoja
na wageni wataingia Tanzania kutokana na visa za Kenya chini ya Itifaki hiyo.
8.1 Mkutano wa Mabalozi wa Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika, wizara
inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1
kwa ajili ya kufanikisha mkutano wa mabalozi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 , na
wizara iliwasilisha maombi ya fedha hizo Hazina kama sehemu ya kipaumbele
lakini hazikuweza kupatikana .
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni,
inaitaka serikali kuiondoa aibu hii na kutenga hizo fedha kwa ajili ya
kufanikisha mkutano huo na tunapendekeza kuwa katika fungu la protocol safari
za nje ndipo fedha hizo zipunguzwe na kutumika kwa ajili ya mkutano wa mabalozi
wetu ili waweze kupeana ushauri na uzoefu,ili kuboresha ufanisi wa majukumu
yao.
8.2 Utaratibu wa Kupeleka Fedha kwenye
Balozi
Mheshimiwa Spika, kutokana
na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye balozi zetu kuwa na mlolongo mrefu wa kwanza
kutoka Hazina na kupelekwa Wizarani, ndipo wizara isambaze fedha hizo kwenye
balozi zetu mbalimbali umesababisha fedha kuchelewa kufikishwa kwa wakati
kwenye balozi zetu na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa na ucheleweshaji wa
kazi kwenye balozi zetu.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaitaka serikali kubadilisha utaratibu huu na hazina iwe inapeleka fedha hizo
moja kwa moja kwenye balozi husika badala ya kuzipitisha wizarani kama
ilivyofanya kwenye fedha za Halimashauri mbalimbali nchini ili kupunguza
usumbufu huo.
Mheshimiwa Spika, baada
ya kusema hayo kwa niaba ya kambi rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
________________________________
Ezekiah Dibogo Wenje
MSEMAJI
MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI
KIVULI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Imesomwa
leo, tarehe 30 Mei, 2013.
No comments:
Post a Comment