TUTAFANYA MAANDAMANO KWENDA WIZARA YA MAJI TAREHE 16 MACHI 2013; NIMESHAWASILISHA NOTISI, TUENDELEE NA MAANDALIZI
Tarehe 16 Machi 2013 nitaongoza
maandamano ya amani ya wananchi kwenda kwa Waziri wa Maji kusimamia uwajibikaji
kuwezesha hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na
ushughulikiaji wa majitaka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Wote mlioshiriki mkutano wa tarehe 10
Februari 2013 (Kwa wale ambao hamkushiriki mnaweza kutazama video hii: http://www.youtube.com/watch?feature=player_embedded&v=O0txSoHqfGY) , mtakumbuka tulimpa wiki mbili Waziri kujitokeza kwa wananchi kujibu hoja
alizokwepa kujibu bungeni.
Tutakusanyika kata ya Manzese eneo la
Bakhresa (jirani na daraja) saa 5 asubuhi na tutapita barabara ya Morogoro
kuelekea kata ya Ubungo zilipo ofisi za Wizara ya Maji kufuatilia majibu ya
ukweli na ukamilifu kuhusu hatua tisa za haraka za kuboresha upatikanaji wa
majisafi na ushughulikiaji wa majitaka nilizopendekeza kwa niaba ya wananchi
bungeni kupitia hoja binafsi na masuala mengine ambayo wananchi watataka
yatolewe majibu siku hiyo.
Kila mmoja anaweza kuendelea na
maandalizi ya kushiriki kwa kuwa tayari tarehe 4 Machi 2013 nimewasilisha
notisi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni na Maafisa wa Polisi Wasimamizi
wa Maeneo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 43 cha Sheria ya Jeshi la
Polisi na Huduma Saidizi Sura ya 322 (The Police Force and Auxiliary Service
Act, Chapter 322).
Itakumbukwa kwamba baada ya kutoa wiki
mbili Waziri alijitokeza mara tatu ndani ya wiki hizo; mbili kati ya hizo ikiwa
ni kupitia mikutano ya CCM na mara moja ikiwa ni kwenye mkutano kati yake na
wafanyakazi wa DAWASA na DAWASCO.
Katika mkutano wa hadhara wa CCM
uliofanyika Temeke mwisho tarehe 16 Februari 2013, Waziri hakutoa majibu badala
yake alirudia tena maelezo yale yale potofu aliyoyatoa bungeni tarehe 4
Februari 2013.
Kwenye mkutano wa hadhara wa Goba tarehe
17 Februari 2013 ambapo aliahidi maji kutoka tarehe 20 Februari, 2013 ambayo
hayakutoka. Tarehe 23 Februari 2013 nilifanya mkutano Goba na kutangaza namba
zake za simu wananchi wamhoji ahadi hiyo na kutaka Manispaa, DAWASA na DAWASCO
waweke kambi Goba mpaka maji yatoke.
Shinikizo hilo limesaidia baadhi ya
maeneo ya Goba maji yameanza kutoka hata hivyo maeneo mengi bado hali ambayo
inahitaji hatua za haraka nilizopendekeza bungeni kuhusu kata hiyo ziweze
kutekelezwa.
Kupitia mkutano wake na DAWASA na DAWASCO
tarehe 21 Februari 2013 (tofauti na maelezo yake bungeni) alikiri kwamba kuna
upotevu wa maji ikiwemo kwa wizi, kuna biashara haramu yenye kuhusisha hujuma
ya miundombinu, bei ya juu ya maji na kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji
katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, zaidi ya wiki moja imepita
Waziri wa Maji na Wizara kwa ujumla haionyeshi kwa matendo kuisimamia kwa
karibu EWURA, DAWASA, DAWASCO na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka
ambazo nilizieleza kwenye hoja binafsi.
Hivyo, wote mlioahidi kupitia mkutano wa
tarehe 10 Februari 2013 kushiriki maandamano na wote ambapo mnaguswa na
matatizo ya maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar Es
salaam tukusanyike Manzese tarehe 16 Machi 2013 saa 5 asubuhi tuandamane kwenda
Wizara ya Maji kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara za 8, 18, 20 na 21.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
05/03/2013
No comments:
Post a Comment