Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, March 1, 2013

NCHI KUINGIA GIZANI, TANESCO YADAIWA KUENDESHWA KISIASA


NCHI iko hatarini kuingia gizani wakati wowote kutokana na hali ya uzalishaji umeme kuwa tete katika Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO), Tanzania Daima imedokezwa. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu ndani, hali ya shirika kifedha ni mbaya licha ya serikali kukwepa kukiri uwepo wa mgawo ikihofia kubanwa kwa ahadi yake kuwa mgawo utakuwa historia. Julai 28 mwaka jana, wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa wizara hiyo, Prof. Sospeter Muhongo, na Naibu wake, George Simbachawene, walilihakikishia Bunge kuwa mgawo wa umeme ungelikuwa historia. Lakini kwa takriban wiki nzima sasa, umeme umekuwa ukikatika hovyo kwa muda mrefu katika maeneo mengi nchini huku TANESCO ikitoa sababu za kawaida kuwa hali hiyo inatokana na matengenezo madogo kwenye nguzo.

TANESCO linadaiwa kuendeshwa kwa hasara kila siku na hivyo kuwa na deni kubwa ambapo sasa mashirika yanayoliuzia umeme yanatishia kusitisha kuendelea kutoa huduma hiyo. Mathalan Songas imeshatishia kusitisha huduma hiyo baada ya deni lake kufikia zaidi ya sh bilioni 80 zinazopaswa kulipwa na TANESCO.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa kwa sasa TANESCO inaendeshwa zaidi kisiasa badala ya ufanisi wa kuliwezesha kujikwamua na kujiendesha ili kuiondolea serikali lawama kwa wananchi. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa TANESCO katika kujinasua isifilisike iliiangukia Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura) kuomba iruhusiwe kupandisha bei ya umeme ili liweze kujiendesha na kunusuru nchi isiingie gizani.


Hata hivyo, kwa maslahi ya wakubwa kisiasa inaelezwa kuwa Wizara ya Nishati na Madini iligundua kuwa suala hilo lisingeiacha serikali salama kutokana na ahadi yake bungeni kuwa mgawo wa umeme ungelikuwa historia. Hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, aliandika barua kuiomba Ewura isikubali ombi la kupandisha bei ya umeme na kuiasa TANESCO kuondoa barua hiyo, na kikao cha bodi ya Ewura cha Januari 24 mwaka huu kilikubali kuiondoa. Baada ya Ewura kukubali ombi la wizara kutokukubali ombi la TANESCO, Maswi ananukuliwa katika waraka mmoja akimshukuru Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu. Waraka huo ulisomeka: “Naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa uungwana wako na kuamua kazi kwa kulinda heshima ya serikali yetu. Heshima haina duka. Nakushukuru sana na naomba tuendelee kuisaidia serikali yetu pamoja na matatizo yaliyo mbele yetu. Kwa aina hii ya kushirikiana tutafika tu wala haina gogoro.”

Chanzo chetu kinasema kuwa baada ya kutopandisha bei ya umeme, serikali kupitia Maswi iliwasiliana na Benki ya Dunia ili iweze kupatiwa mkopo kusaidia shughuli za uendeshaji wa TANESCO kwa ruzuku. Inaelezwa kuwa benki hiyo ilipokea barua lakini ilikataa kutoa mkopo huo kwa masharti kwanza ya kujua mapato na matumizi ya TANESCO kwa mwezi, kiwango cha umeme unaogawiwa, makusanyo halisi na mtiririko wa fedha. Kupitia mawasiliano kati ya Maswi na Jacques Morriset, mchumi mkuu wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Mashariki, mkakati huo haukufanikiwa nandiyo maana shirika hilo bado linadaiwa. Kwa sasa serikali inahaha kutafuta fedha kwa njia zozote mahali popote ili kujinusuru na hali ya ahadi yake kuwa mgawo utakuwa historia. Muhongo na Simbachawene walilieleza Bunge kwamba waligundua kuwa mgawo uliokuwepo kipindi cha nyuma ulikuwa biashara ya watendaji wa TANESCO, waliokuwa wakitumia mwanya huo ili kujineemesha kupitia ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo.
Wataalamu wa masuala ya nishati wanasema kuwa ili mgawo wa umeme utoweke, sh bilioni 42 zitapaswa kutumika kila mwezi kwa ajili ya kuyalipa makampuni yanayoiuzia TANESCO umeme.

Kwa muda mrefu sasa TANESCO imeelezwa kuwa hoi kifedha licha ya kuwa na makusanyo makubwa lakini fedha hizo zimekuwa zikiishia mikononi mwa mafisadi na hivyo shirika kubakia tegemezi kwa serikali. Kwa mujibu wa takwimu za Waziri Muhongo, alizozitoa bungeni wakati akihitimisha hoja ya hotuba ya bajeti kwa mwaka 2012/2013, TANESCO inakusanya mapato kati ya sh bilioni 60 mpaka 70 kwa mwezi. Hata hivyo katika hali ya kushangaza, licha ya matumizi ya shirika hilo kuwa sh bilioni 11 kwa mwezi, waziri alishindwa kufafanua ni wapi zinakwenda sh takriban bilioni 40 zinazosalia. Mara kadhaa Muhongo, naibu wake na TANESCO wamenukuliwa wakikanusha kuwa hakuna mgawo wowote wa umeme kwa sababu shirika limejipanga kutafuta vyanzo vingine vya kuzalisha umeme wa uhakika.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa katika kila sh 100 ambazo TANESCO inakusanya, sh 86 zinakwenda kulipa madeni ya mikataba iliyosainiwa kifisadi ya Aggreko, Symbion, Songas na IPTL.

Mpaka sasa Symbion inalipwa sh milioni 152 kila siku kama gharama za uendeshaji wakati IPTL inalipwa sh bilioni tatu kila mwezi na Songas sh bilioni 4.5. “Agrreko wanaiuzia TANESCO umeme kwa senti dola 42 kwa unit moja halafu TANESCO inauza umeme huo kwa senti dola 11 kwa unit moja,” kilisema chanzo chetu. Serikali ilikataa kununua mitambo ya Dowans wakati huo ikiuzwa kwa dola milioni 59 kwa madai kuwa sheria ya manunuzi ya umma inakataza.
Lakini mitambo hiyohiyo ilinunuliwa baadaye na Symbion kwa dola milioni 159 na sasa kampuni hiyo inazalisha umeme na kuiuzia TANESCO.

Source: Tanzania Daima (March 1, 2013). Nchi kuingia gizani: Tanesco yadaiwa kuendeshwa kisiasa. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: