Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, March 27, 2013

Chadema wajazwa mamilioni



Ni fedha za kuwanoa vijana, wanawake

Zinatoka Denmark, zitasambaa kila kona




Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezidi kuongezewa uwezo, baada ya ‘kumwagiwa’ Sh. milioni 400 na Chama cha Conservative People’s (CPP) cha nchini Denmark. Fedha hizo zimetolewa na chama hicho kwa ajili ya kuwezesha programu ya mafunzo itakayotolewa kwa vijana na wanawake zaidi ya 30,000 wa Chadema ili kuwajengea uwezo wa kisiasa kupitia mafunzo yatakayotolewa na wataalamu wa Chadema na wa kutoka Denmark. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana 9,000 na wanawake 9,000 katika awamu ya kwanza. Dk. Slaa alisema awamu ya kwanza ya programu hiyo itatekelezwa kati ya Machi-Desemba, mwaka huu na ya pili itakuwa kuanzia mwakani. Makubaliano ya ushirikiano wa uendeshaji wa programu hiyo yalitiwa saini katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Makao Makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam jana. Yalisainiwa na Dk. Slaa kwa upande wa Chadema, na Mratibu wa Miradi wa CCP, Rolf Aagaard-Svendsen, kwa niaba ya chama chake. Utiaji saini mkataba huo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chama hicho, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, Naomi Kaihula.
 
Wengine ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema, Victor Kimesera; Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila na Ofisa Mwandamizi wa Habari na Uenezi, Erasto Tumbo. Wengine ni Mkurugenzi wa Halmashauri na Masuala ya Bunge wa Chama hicho, John Mrema; na Mbunge wa zamani wa Denmark, ambaye ni mwanachama wa CCP, Helle Sjelle. Dk. Slaa alisema kimsingi, mkataba huo unalenga maeneo mawili; ya vijana kwa maana ya Bavicha na wanawake kwa maana ya Bawacha. Alisema kinachotaka kufanyika kupitia msaada huo ni kujenga mfumo wa kuwawezesha viongozi wote wa Bavicha na Bawacha kuanzia ngazi ya taifa, kanda na jimbo. Alisema mafunzo makubwa kama hayo, ambayo yanashuka hadi katika ngazi ya jimbo, hayajawahi kufanyika katika historia ya uhai wa Chadema. “Na kwa ujumla wake katika nchi nzima, tunalenga msaada huu kuwafunza viongozi vijana wapatao 9,000 na zaidi, na akina mama viongozi wa Bawacha wapatao 9,000 na mamia vilevile,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
 
“Kwa hiyo ni mpango mkubwa, ambao unaanza Machi hii hii na utaenda mpaka mwishoni mwa Desemba. Awamu ya pili itaanza mwaka kesho.”  lisema Chadema imekuwa ikituhumiwa kuwa imekuwa ikipokea fedha kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuitisha maandamano ya kuipinga serikali. Dk. Slaa alisema tuhuma hizo zimekuwa zikienezwa na baadhi ya maofisa wa serikali, ambao wanawajua. Alisema maofisa hao wamekuwa wakifuatilia nyendo za Chadema na baadhi ya viongozi wake, akiwamo yeye kwa nia mbaya ya kukihujumu chama hicho. “Waendelee kutuhujumu. Maana wananizunguka kila siku hapa na tunawajua,” alisema Dk. Slaa. Hata hivyo, alisema tofauti na madai hayo, Chadema na CCP ni wanachama wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU), ambao lengo lake kuu ni kuhakikisha ustawi wa demokrasia na mfumo wa vyama vingi duniani. Kutokana na hali hiyo, alisema fedha hizo hazikutolewa kwa lengo lingine zaidi ya kuhakikisha ustawi wa demokrasia nchini.
 
Pia alikanusha madai potofu ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya watu wanaoihusisha Chadema na ugaidi, akisema mkataba huo umefanyika wazi na kwa kufuata maadili yote.  Mratibu wa Miradi wa CCP, Rolf alisema wamefurahishwa na utendaji wa Chadema katika kuzungumzia matatizo yanayowakabili wananchi. Alisema kwa utendaji huo mzuri wa Chadema ndiyo maana wameamua kuiunga mkono kwa kuwasaidia fedha hizo. Rolf alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Denmark ya kuvisaidia vyama vya siasa vya nchi zinazoendelea.  Naye Mwenyekiti wa Bavicha, Heche alisema msaada huo ni fursa kwao ya kufundisha vijana na kuwaandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao. “Maana vijijini wamekuwa wakitishiwa kwa sababu hawajui haki zao,” alisema Heche na kuongeza: “Programu hii itatusaidia kupata wagombea kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa na Uchaguzi Mkuu ujao.” Novemba 17, mwaka juzi, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, pamoja na mambo mengine, alidai Chadema imekuwa ikitoa vitisho vya kuandamana na kwamba, wapo tayari kufa kwa ajili ya katiba kutokana na ahadi ya fedha walizopewa na Ujerumani.
 
Lusinde alisema hayo wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011, bungeni, mjini Dodoma. Pia Agosti 12, mwaka jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alikaririwa akidai kuwa anao ushahidi kwamba Chadema imekuwa ikiwahadaa wananchi kwa kuwachangisha fedha, huku ikipokea mabilioni ya Shilingi kwa wafadhili kutoka nje. Nape pia alidai kuwa upo uwezekano wa Chadema kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani. Vilevile, alidai kuwa Chadema inawalaghai wananchi, ina viongozi wasio waaminifu na kwamba iko tayari kuuza nchi kwa uroho wa madaraka. Alitoa kauli hizo wakati Chadema kilipokuwa kinachangisha fedha kutoka kwa wanachama wake kwa ajili ya operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C). Kufuatia kauli hizo, Bodi ya Wadhamini wa Chadema iliagiza wanasheria kumwandikia barua Nape kumtaka kukiomba radhi chama hicho. Baadaye, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alikaririwa akisema kuwa tayari Nape ameshaandikiwa barua ya kisheria Agosti 24, mwaka jana ya kumtaka aombe radhi na kulipa fidia ya Sh. bilioni 3 kwa matamshi hayo aliyoyaita kuwa ni ya uzushi na uongo. 

Source: Saidi M. (March 2013).CHADEMA wajazwa mamilioni. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

No comments: