BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limewatumia waraka viongozi wake wote wa mikoa na wilaya, unaowataka kujiandaa na maandamano ya kushinikiza viongozi wa juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wakiongozwa na Waziri Dk Shukuru Kawambwa, kujiuzulu. Pamoja na kushinikiza viongozi hao kujiuzulu, Bavicha pia inaitaka Sserikali kutangaza matokeo hayo ni janga la Kitaifa na kuiweka elimu kipaumbele cha kwanza katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/14.
Hatua hiyo imekuja siku kadhaa baada ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, uliofanyika kote nchini mwaka jana. Matokeo hayo yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Kawambwa ambaye alisema zaidi asilimia 60.6 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamepata sifuri. Waraka huo ambao Mwananchi ilifanikiwa kuupata jana ukiwa umesainiwa na Katibu Mkuu wa Bavicha,Deogratias Munishi, unawaagiza viongozi hao kufanya maandalizi ya haraka ili kujiandaa na maandamano kama Dk Kawambwa hatajiuzulu wiki moja ijayo.
“Kwa waraka huu ndugu viongozi, mnaombwa kufanya yafuatayo; kuanza maandalizi ya maandamano haya ya kudai elimu bora kwa vijana wa Tanzania, na pia hatma ya waliofelishwa na Serikali ya CCM kwa kuwasiliana na hao waliofeli katika maeneo yenu ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha sahihi zao kama sehemu ya wao kuthibitisha kuitaka Serikali iwajibike” ilisema sehemu ya waraka huo. Waraka huo pia umewataka viongozi hao kuwahamasisha wananchi kuunga mkono azimio hilo kwa kuwaelimisha vijana na wazazi wao kupitia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara na vikao vya ndani. Akizungumzia waraka huo, Munishi alisema huo ni mwanzo wa utekelezaji wa azimio alilolitoa hivi karibuni la kuaanda maandamano.
Source: Dausen Z. (March 1, 2013) BAVICHA Dar yapania kumbana Kawambwa. Retrieved from Mwananchi
No comments:
Post a Comment