Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, February 26, 2013

WAHUNI WAGAWANA MALI ZA CCM


*Waziri Lukuvi, vigogo UVCCM wataharuki

Mjumbe wa balaza kuu la UVCCM,
Willium lukuvi


KUNDI la ‘wajanja’ linaloundwa na watu wasiojulikana, linaendesha mkakati wa kupora kwa njia ya hila viwanja ambavyo ni mali ya Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mtanzania Jumatano limebaini. Habari kutoka ndani ya UVCCM, CCM na kutoka miongoni mwa viongozi waandamizi serikalini, zinaeleza kwamba harakati hizo za kupora mali za jumuiya hiyo, zinachochewa na hofu ya makada wa chama hicho kupoteza nafasi za uongozi walizonazo mara baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Kwa mujibu wa habari hizo, tayari viwanja zaidi ya 100, vilivyokuwa mali za jumuiya hiyo vimekwishatwaliwa na wahuni hao ambao miongoni mwao wanatajwa kuwapo vigogo waandamizi wa CCM.
Mmoja wa wapasha habari wetu anaeleza kwamba, kupatikana kwa taarifa hizo kunatokana na vita ya kugawana mali za CCM inayopiganwa na viongozi na baadhi yao wanadaiwa kueleza kuwa iwapo uchaguzi mkuu wa 2015 utakuwa mbaya kwao, mali zinazomilikiwa na chama hicho zitataifishwa na watawala wapya. Viwanja hivyo ambavyo awali vilikuwa vikikusudia kujengwa nyumba za watendaji wa chama hicho pamoja na ofisi, viko eneo la Mtoni Kijichi, Dar es Salaam. Chanzo kingine cha habari kimelieleza Mtanzania Jumatano kwamba, vita ya kugombea mali za chama kwa sasa ni kubwa ambapo baadhi ya viongozi wanaohusika katika sakata hilo, kila mmoja kwa nafasi aliyonayo amekuwa akijitwalia mali zilizo chini ya usimamizi huo kwa kubadilisha hati na wengine kuzinunua kwa bei ya chee.

Habari ambazo Mtanzania Jumatano limezithibitisha zinaonyesha kuwa, mali ambazo zimekuwa zikichukuliwa ni zile zinazomilikiwa na UVCCM pamoja na za Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Wanawake, (UWT). Viongozi wa UVCCM waliozungumza na Mtanzania Jumatano wamethibitisha kuwa baadhi ya mali za chama hicho sasa hazijulikani zilipo, hata hivyo hawakuwa tayari kulizungumzia kiundani suala hilo kwa maelezo kuwa upotevu wa mali hizo haujathibitika. 

Mwenyekiti wa UVCCM, Sadif Juma Khamis, alipoulizwa iwapo anazo taarifa za mali za jumuiya hiyo kutwaliwa na vigogo, alisema taarifa hizo hazijamfikia kwa sababu yeye bado ni mgeni katika uongozi. Alisema hana taarifa kuwa UVCCM ilikuwa na viwanja zaidi ya 100 ambavyo vimekwishachukuliwa na vigogo, ingawa aliahidi kuzifanyia kazi taarifa hizo alizoziita nzito kabla ya kuweka bayana ukweli utakaogundulika. “Nashukuru sana kwa kunipatia taarifa hizo, nitazifuatilia na ukweli nitakaogundua nitauweka hadharani. Tangu niingie madarakani sijawahi kuonyeshwa mali zozote za jumuiya.  “Ninaomba wana CCM wenye mapenzi mema na UVCCM, wakibaini madudu mengine wanipatie taarifa,” alisema Khamisi ambaye pia ni Mbunge wa Donge (CCM).

Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema ana fahamu kuwepo kwa viwanja hivyo na kwamba ni mali ya jumuiya hiyo, lakini hajapata taarifa iwapo vimekwishaporwa na wakubwa. Alilitaka gazeti hili kumpa muda wa kukagua mali za jumuiya na usalama wake mahali zilipo kabla ya kutoa taarifa rasmi. “Kiujumla sijasikia kama kuna viongozi wetu wamejigawia lakini ngoja kwanza nilifuatilie nitakupa majibu,” alisema. Kwa upande wake mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa UVCCM ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu), William Lukuvi, alieleza kuwa, anafahamu uwepo wa viwanja hivyo kwa sababu ndiye aliyevitafuta na kuvikadhibi kwa uongozi wa jumuiya hiyo.

Lukuvi ambaye amepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, alilieleza Mtanzania Jumatano kwamba, katika siku za karibuni alipata taarifa kuwa vimeporwa na wakubwa. Mwanasiasa huyo alisema, amesikitishwa na taarifa hizo kwa sababu alitumia muda na nguvu zake nyingi kuhakikisha viwanja hivyo vinapatikana kwa kuwashawishi baadhi ya viongozi kufanikisha upatikanaji wake. Alisema baada ya kufanikisha kazi hiyo aliondoka jijini Dar es Salaam kwa uhamisho wa kikazi kwenda mkoani Kagera, baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba. “Mimi ndiye niliyevitafuta hivyo viwanja kati ya mwaka 1991 au 1992 na baada ya kuvipata nilikabidhi vyote zaidi ya 100 na hati zake kwa uongozi wa UVCCM kisha nikaondoka kwenda Kagera ambako nilikuwa nimeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba.

“Nakumbuka UVCCM ilipata viwanja hivyo wakati Kitwana Kondo akiwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, lakini hivi karibuni nimesikia kuwa wapo wakubwa ndani ya chama wamekwishajimilikisha. Waulizeni viongozi wa jumuiya watawaambia ni akina nani waliovipora.” Lukuvi alipoulizwa hatua zilizochukuliwa na Baraza la Wadhamini la UVCCM, ambalo yeye ni mjumbe wake kudhibiti uporaji huo, alisema wakati taarifa za kuporwa kwa viwanja hivyo zinapatikana yeye alikuwa hajateuliwa kuwa mjumbe wa baraza hilo.

Source:Mushi G. (February 27, 2013). Wahuni wagawana mali za CCM. retrieved from Mtanzania

No comments: