KAMPUNI ya Game Frontiers Tanzania (GFT) inayojishughulisha na uwindaji wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na Kikosi cha Askari Wanyamapori katika Pori la Akiba la Selou, wamefanikiwa kukamata pembe za ndovu zenye thamani ya dola za Kimarekani 120,000 sawa na sh milioni 192 za Kitanzania. Kaimu Mkuu wa Pori la Akiba Kanda ya Kusini Magharibi Likuyuseka, Bernald Lijaji, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Februari 17 mwaka huu majira ya asubuhi, huko katika maeneo ya Jumuia ya Mbarang’andu. Lijaji alisema pembe zilizokamatwa zilikuwa 15 zenye thamani ya fedha hizo, risasi tisa na bunduki mbili kati ya hizo moja ni aina ya Gobole na nyingine Raifo.
Aidha aliwaambia waandishi wa habari kuwa pembe hizo na bunduki zilizokamatwa hivi sasa zinashikiliwa katika ofisi ya Selou iliyoko wilayani Namtumbo na kwamba majangili waliokurupushwa na nyara hizo wametokomea kusikojulikana. Alifafanua kuwa pembe hizo zilizokamatwa ni sawa na tembo wanane waliouawa, ambapo vitendo vya ujangili huo vimekuwa vikiwatesa kutokana na watu wasiokuwa waaminifu kuingia ndani ya pori na kuua wanyama bila kufuata taratibu na sheria za nchi. Awali alieleza kuwa jitihada za kuwakurupusha majangili hao zinatokana na ushirikiano uliopo kati ya kampuni ya GFT, askari wa uhifadhi wa vijiji (VGS) na kikosi cha askari wanyamapori.
Mafanikio hayo yalitokana na kampuni ya GFT kuwezesha kutoa mafuta na gari ya doria, chakula, mawasiliano na kuwalipa posho askari ambao hushughulika katika kazi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, mwakilishi wa kampuni hiyo inayojishughulisha na uwindaji katika pori la Mbarang’andu wilayani Namtumbo, Mohamed Mpapa, alisema mafanikio hayo yanatokana na jitihada walizonazo na ushirikiano na wananchi walio jirani na pori hilo. Hata hivyo Mpapa alitoa wito kwa jamii kuendelea kujenga ushirikiano katika kuwafichua watu wanaohusika na vitendo vya ujangili wa kuua wanyama walio katika hifadhi na kutorosha nyara za serikali pasipo kufuata taratibu zilizowekwa na nchi.
Source: Konala J. (February 22, 2013) Shehena nyingine ya pembe za ndovu yanaswa. Namtumb. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment