NCHI IMEINGIA TENA KWENYE MGAWO WA UMEME, SERIKALI IELEZE WANANCHI UKWELI NA HATUA KUHUSU UDHAIFU KWENYE UTEKELEZAJI WA MPANGO WA DHARURA
Nchi imeingia tena
katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na Waziri wa Nishati na
Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28 Julai 2012.
Hali hiyo ni matokeo
ya Serikali kutozingatia tahadhari niliyoitoa bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kwa nyakati mbalimbali kwa nafasi yangu ya
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini juu ya hali tete iliyotarajiwa kuwepo na
hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa
umeme.
Ikiwa ni sehemu ya
wajibu wa kibunge wa kuisimamia Serikali nawataka viongozi na watendaji wa Wizara
ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuacha kuficha hali
ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na
hatua za haraka zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Iwapo Wizara na
TANESCO hawatatoa matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa nafasi yangu ya Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya mgawo wa umeme uliojitokeza
ili hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu ambapo wajumbe wa kamati ya nishati na
madini wenye wajibu wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya Bunge katika sekta hizo
nyeti hawajateuliwa.
Aidha, pamoja na kutoa
maelezo kuhusu mgawo wa umeme, Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO watumie
nafasi hiyo pia kueleza hatua zilizochukuliwa kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili
kuhusu tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa vifaa na uzalishaji wa umeme wa
dharura ikiwemo kuhusu mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua
umeme.
Ikumbukwe kwamba
mwanzoni mwezi Agosti 2012 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT)
iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa hesabu za Shirika la Umeme
(TANESCO) kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zilitajwa bungeni na
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
tarehe 27 Julai 2012 na Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya
hoja ya Serikali tarehe 28 Julai 2012.
Wizara ya Nishati na
Madini na TANESCO waeleze pia hatua iliyofikiwa kuhusu uchunguzi mwingine
uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuanzia mwezi
Agosti 2012 wa mchakato wa ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya
kufua umeme wa dharura kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotolewa bungeni
kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27
Julai 2012 liundiwe kamati teule ya Bunge ili uchunguzi wa kina uweze
kufanyika.
Wenu katika uwakilishi
wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini
27 Februari 2013
No comments:
Post a Comment