WANANCHI wa Mtwara wametoa masharti mazito wakiitaka serikali iyatekeleze kwanza kabla ya kuanza kuchimba gesi asili na kuisafirisha kwa njia ya bomba kwenda eneo Kinyerezi jijini Dar es Salaam. Wakizungumza na Tanzania Daima mkoni humo hivi karibuni, baadhi ya wananchi hao walisema kuwa sakata la gesi bado ni tete, na hivyo kuonya kuwa serikali inapaswa kutafakari upya badala ya kutumia nguvu na upotoshaji. “Tunatambua gesi hii ni rasilimali ya Watanzania wote, lakini mikoa ya kusini imesahaulika, na huu ndiyo msimamo wa wananchi wa mikoa hii bila kujali itikadi za kisiasa. Gesi hii haitatoka bila serikali kuendeleza mikoa yetu,” alisema mmoja wa wananchi hao. Katika masharti hayo, wanataka kwanza serikali ikamilishe ujenzi wa barabara ya Mtwara-Dar kwa kiwango cha lami, ujenzi ambao wanadai umekuwa ukisuasua kwa miaka mingi, na hivyo kuleta shaka kama gesi itaondoka bila miundombinu hiyo kukamilika, ni dhahiri watasahaulika kabisa.
Pili, wanahitaji kujengewa uwanja wa ndege wa kisasa wenye kuruhusu kutua ndege kubwa ili kuwavutia watalii na wawekezaji kuwekeza huko pamoja na kupanuliwa kwa bandari ya Mtwara, jambo wanalodai litawapa nafasi ya kusafirisha bidhaa zao kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi kirahisi. “Unajua serikali ndiyo iliua viwanda vyetu vya korosho hapa Mtwara, ikaleta wawekezaji kuchimba gesi Kilwa, halafu wakauacha mji huo hauna umeme. Sasa tumeona ya Kilwa, hatuwezi kuacha gesi iende bila kuwekewa viwanda, umeme wa uhakika na kufufua bandari yetu,” aliongeza mwananchi mwingine. Tanzania Daima ilibaini kuwepo pia kwa msigano mkubwa kati ya wananchi na viongozi wa vyama vya kisiasa walioratibu na kuongoza maandamano ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam yaliyofanyika Desemba 27, mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa wamewashtukia viongozi hao wa kisasa, kwani wamekuwa wanafiki na wenye tamaa ya fedha baada ya kuketi na kulainishwa na serikali. “Hatuwahitaji wanasiasa kwa sasa maana tumegundua wana ajenda zao za kutaka kujinufaisha kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu 2015. Sisi kauli yetu ni gesi kwanza, siasa baadaye. Wenzetu hawa walikwenda Dar es Salaam wakakutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, na sasa wanazungumza lugha za serikali. Hapa gesi haitoki,” alisema mmoja wa wananchi hao. Tanzania Daima ilitaka kufahamu ikiwa hawaoni watachelewa kupata maendeleo kutokana na msimamo wao huo, lakini majibu yao yalikuwa wazi kwamba kama serikali haijajiandaa kuchimba rasilimali hiyo kwa ajili ya watu wake basi iache, maana haiozi. “Hayati Mwalimu Julius Nyerere kila mara alikuwa anasema kuwa aliacha kuchimba madini kwa vile watu wetu hawakuwa wameandaliwa ili wanufaike. Yalikaa miaka yote ardhini bila kuoza, hivyo hata gesi imekaa miaka yote haijaoza kama hawawezi kutunufaishi waiache,” alisisitiza mwananchi huyo.
Licha ya mikutano na maandamano ya kisiasa kuzuiliwa kwa muda na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Tanzania Daima limedokezwa kuwa wananchi hao kwa sasa wanaendesha mikakati yao kupitia mikutano ya siri ambayo inafanyika kwa ulinzi mkali. Kwamba kwa siku wanafanya vikao visivyopungua vitano ili kupanga mikakati ya kuhakikisha hawasalitiani na kuruhusu gesi hiyo kuondoka bila matakwa yao kutekelezwa. “Katika vikao vya karibuni tayari tumefikia uamuzi wa kuunda kikosi kazi cha vijana, ambacho kimepewa jukumu la kuzunguka eneo zima la gesi ili kuhakikisha hakuna bomba linalotandazwa na serikali kwa kushirikiana na wawekezaji inaotaka wachimbe rasilimali hiyo,” kilisema chanzo chetu.
Source: Kamukara E. (February 25, 2013). Mtwara watoa masharti mazito. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment