ASEMA HAINA SIFA YA KUITWA HOSPITAL YA RUFAA
MBUNGE wa Ilala, Azan Zungu (CCM), amekosoa uamuzi wa Serikali wa kuipa Hospitali ya Amana iliyopo jijini Dar es Salaam, hadhi ya Hospitali ya Rufaa. Mbunge huyo alisema wazi wazi kwamba hospitali hiyo haina sifa ya kuitwa Hospitali ya Rufaa, kutokana na kukabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa na vifaa muhimu. Zungu aliyasema hayo jana, mara baada ya kutembelea hospitali hiyo, huku akiwa ameandamana na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mbunge huyo alisema, uhaba mkubwa wa madaktari unasababisha hospitali hiyo kukosa sifa ya kuitwa Hospitali ya Rufaa. “Madaktari bingwa ni tatizo kubwa katika hospitali hii, hivyo kupelekea kuwa na msongamano wa wagonjwa wengi, hospitali hii pia haina gari la kubebea dawa. “Chumba cha kuhifadhia watoto njiti kina uwezo wa kuhifadhi watoto 27, lakini inafikia wakati mwingine tunahifadhi zaidi ya watoto 50, hii ni hatari. “Suala la dawa ni jambo jingine, tuna uhaba mkubwa wa dawa na kusababisha watu kutoka nje ya hospitali kununua dawa kwa gharama kubwa zaidi,” alisema.
Mbunge huyo alisema ili hospitali hiyo iwe na hadhi hiyo, Serikali inatakiwa kuleta madaktari bigwa, vifaa na dawa za kutosha, vinginevyo itaendelea kubaki kama ilivyo. Kwa upande wake, daktari bigwa wa magonjwa yote, Meshack Shimwela, alisema uhaba wa madaktari uliopo hapa unasababisha kuwa na wagonjwa wengi na kutohudumiwa kwa wakati. “Serikali iangalie kwa makini suala hili, kwani tuko madaktari bingwa wawili na huwa tunashindwa kujigawa,” alisema Shimwela.
Source: Kannonyere Z. (February 26, 2013). Mbunge CCM ainanga hospitali ya Amana. Dar es salaam. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment