Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, February 19, 2013

MATOKEO KIDATO CHA NNE AIBU TUPU

SHULE ZA SERIKALI ZATUPWA NJE KUMI BORA, 24 WAANDIKA MATUSI

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, jana imetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na wa maarifa (QT), ambapo idadi ya waliofeli imeongezeka maradufu tofauti na mwaka jana. Jumla ya watahiniwa 240,903 wa kidato cha nne wamefeli huku wasichana 120,239 na wavulana 120,664 wakipata ziro. Hali hiyo imekuwa tofauti ukilinganisha na 2011 ambapo watahiniwa 156,089 sawa na asilimia 46.41 ya wahitimu wote walifeli mtihani huo kwa kupata ziro.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema matokeo hayo yameonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 456,137 walifanya mtihani huo ambapo kati yao 23,520 ndio waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu. “Watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 480,036 wasichana 217,583 na wavulana 262,453, wasiofanya mtihani walikuwa 21,820 na wa shule walikuwa 411,230 wakati wa kujitegemea walikuwa 68,806, ”alichanganua Waziri Kawambwa.

Kawambwa alisema wavulana 1,073 na wasichana 568 wamepata daraja la kwanza na wavulana 4,456 na wasichana 1,997 walipata daraja la pili. Kwa upande wa daraja la tatu watahiniwa 15,426 kati yao wavulana wakiwa 10,813 na wasichana 4,613. Watahiniwa 103,327 kati yao wavulana wakiwa 64,344 na wasichana 38,983 wamepata daraja la nne. Aidha shule za seminari na watu binafsi zimefanya vizuri ambapo Shule ya Wasichana ya St. Francis ya Mkoa wa Mbeya imeongoza ikifuatiwa na shule ya wavulana Marian ya mkoa wa Pwani. Nyingine zilizofanya vizuri ni shule ya wavulana Feza, shule ya wasichana Marian, Rosmini Seminari, Cannosa, Jude Moshono, St Marys ya Mazinde Juu, shule ya wasichana ya Anwarite na Kifungilo. Kawambwa pia alizitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri kuwa ni Mibuyuni ya Mkoa wa Lindi, Ndame ya Unguja, Namndimkongo ya Pwani, Chitekete ya Mtwara na Maendeleo ya Dar es Salaam. Zingine zilizofanya vibaya ni Kwamndolwa ya mkoa wa Tanga, Ungulu ya Morogoro, Kikale ya Pwani, Nkumba na Tongoni zote za Tanga.


Matokeo yaliyozuiwa

Waziri alisema Baraza la Mitihani limezuia matokeo ya watahiniwa 28,582 ambao hawakulipa ada ya mtihani.
“Watahiniwa ambao hawakulipa ada wanayodaiwa wanatakiwa walipe na faini na ikiwa hawatalipa kwa miaka miwili toka kutangazwa, matokeo yao yatafutwa,” alisema Kawambwa.

Matokeo yaliyofutwa

Kawambwa alisema kuwa jumla ya watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo yao yote ya mitihani baada ya kubainika kufanya udanganyifu ambapo kati yao watahiniwa 624 ni watahiniwa wa shule na wakujitegemea ni 148.

Walioandika lugha chafu

Jumla ya watahiniwa 24 waliandika lugha chafu katika karatasi za majibu ambapo serikali imeeleza kuwa watahiniwa hao hawataruhusiwa kufanya mitihani inayoendeshwa na Baraza la Mitihani kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.

Mtihani wa maarifa (QT)

Watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 21,310 ambapo kati yao wasichana walikuwa 13,134 na wavulana 8,176 kati yao watahiniwa 5,984 ndio waliofaulu

Tathmini ya ufaulu wa watahiniwa

Kwawambwa alikiri kuwa shule zilizofanya vizuri ni zile zilizojitosheleza katika mahitaji ya msingi ikiwemo walimu wa kutosha, miundombinu na vifaa vya kuwafundishia. Pia alisema shule zilizofanya vibaya zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi kukosa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati. “Kutokuwepo kwa maabara na maktaba kwa shule zenye mikondo ya sayansi, walimu kukosekana na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada lakini pia wazazi na walezi kutoshiriki katika kuhakikisha wanasimamia elimu ya mtoto kunachangia ongezeko la kufeli,” alisema Kawambwa. Aidha serikali imeweka mkakati kuhakikisha changamoto hizo zinaondoka kwa kuboresha miundombinu, mgawanyo wa walimu, ukaguzi wa ndani wa mara kwa mara na ruzuku ya sh 25,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya kununua vitabu na vifaa vya shule.

Source: Mnare H. (February 19, 2013) Tanzania Daima. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: