OFISI ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, inadaiwa kuandaa mkakati wa kumfukuza kazi Ofisa Kilimo wa Kata ya Itundula kwa madai kuwa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Evarista Kalalu amefikia uamuzi huo kutokana na kasi ya CHADEMA inayoendelea vijijini na kuwa mwiba kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwamba ili kufanikisha mkakati huo, Kalalu ataongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ili kuwatisha wananchi watakaoonekana kutokupendezwa na uamuzi huo. “Wamepanga kuwapa kesi watu watakaoonekana kuwa wakali kutokana na mambo yatakayoongelewa katika mkutano huo, ikiwemo agenda ya kuuza ardhi ya kijiji kinyemela pamoja na kufukuzwa kwa ofisa kilimo,” kilisema chanzo chetu.
Kwamba mwajiri wa ofisa kilimo huyo amepewa maelekezo ya kutoa tamko la kumfukuza kazi mbele ya wananchi. “Kuna ajenda tatu zitakazozungumzwa leo, lakini lengo kubwa ni kumfukuza ofisa kilimo pamoja na kubomoa tawi la CHADEMA,” kiliongeza chanzo hicho. Mwenyekiti wa CHADEMA katika Kata ya Itandula, Titus Kaduma alisema taarifa za kufukuzwa kwa ofisa huyo katika mkutano wa leo zimezagaa kila kona katika kata hiyo jambo linalowatia wasiwasi wananchi juu ya utekelezaji wa serikali katika masuala muhimu kwa jamii. Alisema mbinu hizo zilianza chini chini, lakini zinajionesha wazi kutokana na mipango yao kushindikana kila wakati. Naye ofisa kilimo huyo, Ngwalanje Emmanuel alipoulizwa, alithibitisha kupata taarifa juu ya kufukuzwa katika mkutano. “Si kila mtu atakuchukia ndugu, lazima utakuwa na rafiki. Taarifa za kunifukuza kazi katika mkutano wa leo ninazo tayari, lakini pamoja na hilo litazungumzwa na suala la ardhi ya kijiji lililoulizwa na watu wanne wa mipango ya fedha na uchumi,” alisema. Alisema kuwa Februari 4 mwaka huu aliitwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kumhoji kwanini anajihusisha na masuala ya siasa. Ngwalanje alisema walimtaka aandike barua ya kuacha kazi jambo alilolikataa na kusema ni unyanyasaji kwa kuwa utaratibu wa kazi anauelewa, na anaufuata. DC Kalalu alipotafutwa kulizungumzia suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake kutokuwa hewani.
Source: Chache G. (February 2013). DC atumia siasa kumng'oa ofisa. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment