SASA ni dhahiri sumu aliyoimwaga Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na makada wengine wa chama hicho mjini Moshi wiki iliyopita, imeanza kukitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jimbo la Moshi Mjini, limekuwa likishikiliwa na kambi ya upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, huku Chadema kikiigaragaza CCM katika kiti cha ubunge mara tatu mfululizo.
Makada wa CCM wamejitokeza na kuhoji ukimya huo wa CCM wakati sumu hiyo imeanza kusambaa kwa kasi miongoni mwa wananchi na kukiweka chama hicho njiapanda uchaguzi mkuu 2015.
Kada wa CCM, Ramadhan Mwindad ‘Gadaffi’ jana alizua kizaazaa katika ofisi za CCM Moshi Mjini, alipoamua kujitoa mhanga na kwenda kuwahoji viongozi sababu za kutojibu mapigo. Tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi, lilisababisha kada huyo na kiongozi mmoja wa CCM ngazi ya wilaya kushindwa kujibu hoja na kudai kada huyo ametumwa na Chadema.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea mbele ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo ambaye pia ni Diwani, Michael Mwita.
“Mimi ni kada wa CCM nimekwenda pale saa 8:00 mchana huu (jana) na kuwauliza kwa nini kila siku mnafanya vikao vya ndani vya kikatiba, lakini hamwendi kwa wananchi kujibu mapigo?”alisema.
Badala yake, kada huyo alisema kiongozi huyo ngazi ya wilaya alimjia juu na kumtuhumu kuwa ametumwa na Chadema kuhoji mambo hayo na kukwepa kabisa kujibu hoja ya msingi.
“Viongozi wa kitaifa wametukanwa na kudhalilishwa sana.Mkuu wetu wa mkoa mpaka imefikia mahali ameitwa ki model (mwanamitindo) bado viongozi wetu wamekaa kimya,”alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na kada mwingine wa CCM Kata ya Longuo, ambaye alisema baadhi ya viongozi walijinadi kwa mbwembwe katika uchaguzi uliopita lakini sasa wanachama hawaoni makeke yao.
“Kuna viongozi walijinadi kwa wapiga kura kuwa oooh hili ni jembe mchagueni, mbona kimya? Hata kujibu tu matusi na kejeli za mkutano ule wa Chadema wameshindwa”alisema kada huyo. Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Elizabeth Minde alipoulizwa jana kuhusu madai ya wanachama wake alisema yuko kwenye kikao na pindi atakapomaliza tu angelipigia gazeti hili kutoa ufafanuzi.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Mwita alipoulizwa kuhusu tafrani hiyo alisema hakuona kama kulikuwa na mabishano katika ofisi hizo za CCM kwa kuwa alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio.
“Nilimwona Gadaffi na (jina la kiongozi wa wilaya) wakizungumza ila sikujua wanazungumzia nini, lakini nataka ifahamike CCM ina utaratibu wake wa kuitisha mikutano na hatujibu matusi,” alisema.
Mwita alisisitiza kuwa kamwe CCM haiwezi kujibu hoja kwa kusukumwa na mikutano ya Chadema bali watafanya hivyo kunapokuwa na hoja na CCM iko katika mchakato wa kujibu mapigo.
Katika mkutano huo, Dk Slaa, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche walimwaga sumu inayokifanya CCM kuweweseka.
Katika mkutano huo viongozi hao pamoja na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema wanadaiwa kutumia maneno makali kumshambulia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.
Viongozi hao wa Chadema waliwachongea Gama, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bernadette Kinabo na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ibrahim Msengi kuwa wanaingilia utendaji wa Halmashauri.
Kauli za viongozi hao zilitokana na hotuba ya Meya wa Manispaa ya Moshi kuwashtaki viongozi hao wa serikali ya CCM kuwa wanazuia utekelezaji wa maamuzi ya baraza kwa masilahi ya kisiasa.
Meya huyo alisema viongozi hao wamekuwa wakitumia vibaya vikao vya ushauri mkoa (RCC) na vile vya wilaya(DCC) kuingilia uamuzi halali wa Manispaa ya Moshi inayoongozwa na Chadema.
Alitoa mfano wa viongozi hao kumwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bernadette Kinabo kuendesha operesheni dhidi ya wafanyabiashara wadogo ili kuichonganisha Chadema na wananchi.
Kwa mujibu wa Meya huyo, Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limekuwa katika wakati mgumu kutokana na Kinabo kukataa kutekeleza maazimio ya vikao halali ili tu kuinufaisha CCM kisiasa.
Mathalan alisema, sera ya Chadema Moshi Mjini ni kuwalipia ada wanafunzi wote wa sekondari ambao wazazi wao hawana uwezo, lakini mkurugenzi huyo amekataa kuidhinisha fedha hizo.
Meya huyo alisema mwaka 2011/2012, Halmashauri hiyo inayoongozwa na Chadema ilitenga Sh196 milioni kulipa ada hizo na mwaka 2012/2013 imetenga Sh216 milioni ambazo zote hazijaidhinishwa.
“Ukimuuliza anasema sera ya elimu bure siyo sera ya Serikali.Tunaomba hoja hiyo uipeleke bungeni tujue ni wakati gani vyama vinaweza kutekeleza sera zake kwa halmashauri inazoziongoza,”alisema.
Meya huyo alisema vitendo vinavyofanywa na viongozi hao wawili ni dhahiri vina lengo la kuidhoofisha Chadema kisiasa katika Jimbo la Moshi na pia kuwagombanisha na wananchi.
Source: Mwananchi (January 26, 2013)
No comments:
Post a Comment