TAARIFA YA KUPELEKA GESI BAGAMOYO ILIAMSHA HISIA ZA WANA MTWARA
MOJA ya mambo yaliyoamsha hisia za wakazi wa Mkoa wa Mtwara hadi kushinikiza kwa vurugu wakitaka gesi isitoke mkoani humo, ni taarifa kuwa nishati hiyo ingepelekwa wilayani Bagamoyo, nyumbani kwa Rais Jakaya Kikwete.Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema jana nyumbani kwake mjini Dodoma kuwa, mbali na imani hiyo, amebaini pia kuwa mpasuko ndani ya CCM mkoani Mtwara na harakati za kisiasa ni sababu nyingine iliyochochea mgogoro huo.
Pinda alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro huo ambao ulisababisha vifo vya watu wanne huku wengine wakijeruhiwa vibaya na uharibifu mkubwa wa mali zikiwamo nyumba za wabunge kuchomwa moto na namna alivyofanikiwa kuuzima.Waziri Mkuu alifanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara, Januari 25 na 26 mwaka huu na kufanikiwa kuzima mgogoro huo baada ya kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya wadau wa gesi mkoani humo.
“Sasa hili nililitolea ufafanuzi kwa kukanusha kuwa siyo kweli kwamba gesi inakwenda Bagamoyo. Lakini pia baada ya kukaa nao nilibaini kuwa hata viongozi wenyewe wa CCM hawako pamoja,” alisema Pinda na kuongeza: “Pamoja na hayo nikachukua maelezo kuhusu matatizo yao mengine na nikawaahidi kwamba nitayafikisha katika mamlaka husika ili waweze kuona namna ya kufanya.”
“Sasa hili nililitolea ufafanuzi kwa kukanusha kuwa siyo kweli kwamba gesi inakwenda Bagamoyo. Lakini pia baada ya kukaa nao nilibaini kuwa hata viongozi wenyewe wa CCM hawako pamoja,” alisema Pinda na kuongeza: “Pamoja na hayo nikachukua maelezo kuhusu matatizo yao mengine na nikawaahidi kwamba nitayafikisha katika mamlaka husika ili waweze kuona namna ya kufanya.”
Madai kwamba gesi hiyo inapelekwa Bagamoyo yalikuwa moja ya ujumbe mkuu uliokuwa umeandikwa kwenye baadhi ya mabango wakati wa maandamano ya Desemba 27 mwaka jana yaliyofanyika Mtwara Mjini, yakiratibiwa na baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani. Pinda alisema viongozi wa kisiasa mkoani Mtwara wakiwamo wabunge, wameonekana kuwa na mpasuko unaosababisha uchochezi kwa makundi ya watu.
Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya Waziri Mkuu, Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Alhaji Masoud Mbengula alikiri chama hicho kumeguka na akataja sababu kuwa ni makundi yaliyotokana na uchaguzi wa ndani uliofanyika mwaka jana. “Tusiwe wanafiki, ni kweli kuna makundi ndani ya chama… wabunge hawako pamoja na ndiyo hali iliyotufikisha hapa… suala hili lipo wazi kabisa,” alisema Alhaji Mbengula.
Kamati ya Spika hatihati
Akizungumzia Kamati ya Bunge iliyotarajiwa kuundwa na Spika kwenda Mtwara kwa ajili ya kuwasikiliza wananchi wa huko, Pinda alisema hawezi kuingilia mhimili huo wa Dola isipokuwa atatoa taarifa bungeni na kama Spika ataona wabunge wameelewa, basi ataamua lolote. “Nitakuwa na nafasi ya kuzungumzia jambo hili ndani ya Bunge na Spika akiona wabunge wamenielewa bila shaka atasitisha lakini akiona bado inafaa ataamua yeye,” alisema.
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari jana, kiongozi huyo alifanya mazungumzo na Mawaziri wanaotoka Mkoa wa Mtwara ambao ni George Mkuchika (Utawala Bora) na Hawa Ghasia (Tamisemi) pamoja na wawekezaji wa kutoka China ambayo alisema yalilenga kuwapa halihalisi ya huko.
Nchimbi afunguka
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema vurugu hizo zimefikia mwisho na Serikali haitavumilia tena machafuko ya aina hiyo. Dk Nchimbi alisema timu ya wataalamu ipo Mtwara kuweka mambo sawa na kusema Serikali itatimiza majukumu yake pasi na shaka yoyote na kusisitiza kuwa haiwezi kukubali Tanzania ikawa vipande. Alisema Serikali inafanya tathmini kujua hali ilivyo Mtwara na ikibidi itasitisha shughuli zote za kisiasa mkoani humo.
Mtwara wampinga
Wakazi wa Mkoa wa Mtwara wamegawanyika baada ya ziara ya Waziri Mkuu baada ya baadhi yao kupinga mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi asilia kwa bomba kwenda Dar es Salaam. Katika ziara yake, Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya manufaa yatakayopatikana mkoani Mtwara kutokana na uzalishaji wa nishati hiyo kiasi cha kumshangilia na kumpigia makofi. Shura ya Maimamu Mtwara imesema jana kwamba haijaridhishwa na majibu iliyoyaita mepesi ya Waziri Mkuu katika hoja nzito na kwamba bado Serikali haijaupatia suluhu mgogoro huo.
“Baada ya kutoka pale tulifanya kikao kupitia maelezo ya Waziri Mkuu, kuna maeneo hatujaridhika … amezungumzia ‘powerplant’ (mtambo wa kufua umeme) kama mtambo wa kusafisha gesi, ndiyo aliousema utajengwa Madimba… lakini sisi tunahitaji ‘powerplant’, mashine za kufua umeme pamoja na hiyo ya kuchakata gesi iwe Mtwara… katika eneo hilo hatujaridhika,” Msemaji wa Shura hiyo, Sheikh Abubakar Mbuki alisema na kuongeza:
“Waziri Mkuu asituambie tu gharama za kutandaza nyaya ni kubwa kuliko bomba la gesi akaishia hapo. Atuambie gharama hizo ni kiasi gani badala ya kusema ni gharama kubwa… mbona gharama za bomba zipo wazi, kwa nini hizi za nyaya hazisemwi?”
Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Katani Katani alisema “Sijaelewa kabisa… nashangaa watu wanashangilia wakati madai yetu ya msingi hayajapata ufumbuzi… dai letu la kwanza lilikuwa viwanda vya kuchakata gesi vijengwe Mtwara, hilo limepatiwa ufumbuzi, la pili lilikuwa mitambo ya kufua umeme Megawati 600 ijengwe Mtwara.”
“Hili hajalipatia ufumbuzi, tunachokataa sisi wana Mtwara ni kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, tunataka mashine zinazojengwa Kinyerezi zihamishiwe Mtwara… kutuambia kupeleka umeme Dar es Salaam kwa njia ya nyaya ni gharama kubwa hilo sikubaliani.” Alisema kutokana na kutopatikana kwa ufumbuzi wa dai hilo moja, bado wananchi wa Mtwara wataendelea kupinga mradi huo.
Akizungumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake juzi, Pinda alisema gesi ghafi haitasafirishwa kwa bomba kwenda Dar es Salaam na badala yake usindikaji utafanyika Mtwara. “Wataalamu wanasema gesi haiwezi kwa namna yeyote ile kusafirishwa kama ilivyo, lazima ibadilishwe kuwa hewa au barafu… kiwanda cha kusafisha gesi kitajengwa Madimba, gesi yote itakayotoka Mnazi Bay itasafishwa hapo na masalia yote yatabaki huku ili kuvutia viwanda vya mbolea na vingine vinavyotumia malighafi hizo,” alisema Pinda na kuongeza:
“Kama tungekuwa tunasafirisha gesi ghafi basi hata kiwanda cha Dangote kisingejengwa hapa… gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme… tusaidieni wenzetu kuliokoa Taifa na tatizo la umeme.”
Source: Chidawali H. na Bakari A. (January 30, 2013). Mwananchi. Dodoma na Mtwara.
No comments:
Post a Comment